Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais Putin asema mapinduzi Mashariki ya Kati hayakuleta chochote ila majanga, vita na umaskini

Rais Putin asema mapinduzi Mashariki ya Kati hayakuleta chochote ila majanga, vita na umaskini

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameeleza kusikitishwa na kuona kwamba baadhi ya nchi ambazo zinalaani vitendo vya kigaidi kutoka vikundi kama vile ISIS, wakati huo huo zinaendelea kufadhili vikundi hivyo na kuvipatia risasi.

Katika hotuba yake leo mbele ya kikao cha 70 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais Putin amesema mapinduzi yaliyotokea Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kuliko kuleta demokrasia na maendeleo, yamesabaisha majanga ya kijamii, umaskini na vita, akiuliza je wale waliosababisha hali hiyo hawatambui walichofanya?

Kuhusu Syria akafananua zaidi:

“Muda wote Urusi imekuwa na msimamo wa kupambana na aina zote za ugaidi. Leo tunawapatia Syria na Iraq usaidizi wa kijeshi na kitaaluma ili kupambana na vikundi vya kigaidi, Tunaamini kwamba ni kosa kubwa kukataa kushirikiana na serikali na jeshi la Syria, ambalo linajitahidi kupambana moja kwa moja na ugaidi.”

Hatimaye Rais Putin amesema Urusi itaendelea kulipigia debe lengo la Umoja wa Mataifa la kuunganisha nchi zenye mitazamo tofauti na kutafuta maelewano licha ya sintofahamu baina ya nchi.