Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Burkina Faso kwa kurejesha utawala wa mpito:Ban

Heko Burkina Faso kwa kurejesha utawala wa mpito:Ban

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha hatua ya kurejeshwa madarakani kwa rais wa serikali ya mpito nchini Burkina Faso, Michel Kafando sambamba na taasisi zake.

Ban katika taarifa yake amesifu jitihada zilizofanikisha hatua  hiyo ikiwemo zile za jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, jitihada ambazo amesema zimewezesha mzozo huo wa kisiasa kupatiwa suluhu haraka.

Halikadhalika amepongeza ushirikiano wa kipekee kati ya Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika na ECOWAS pamoja na wadau wengine akisema wamewezesha kurejea kwa utawala wa kikatiba nchini humo.

Katibu Mkuu amesema kurejea kwa hali hiyo kutawezesha kuendelea kwa mchakato wa kipindi cha mpito nchini Burkina Faso na hatimaye uchaguzi mkuu wa wabunge na Rais kufanyika mwezi ujao kama ilivyopangwa.

Amesema mwakilishi wake maalum kwa Afrika Magharibi Mohamed Ibn Chambas ataendelea kushirikiana na taasisi za kikanda na kimataifa ili uchaguzi huo ufanyike kwa uwazi, huru na amani.