Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu ni mdau katika SDGs, hususan vijana- Ban

Kila mtu ni mdau katika SDGs, hususan vijana- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesisitiza leo umuhimu wa kuwaweka watoto na vijana katikati ya ajenda mpya ya maendeleo endelevu ya 2030.

Ban amesema hayo katika hafla ya kuzindua chombo cha dijitali kitakachowawezesha watoto na vijana kutuma ujumbe wao moja kwa moja kwa viongozi wa dunia, wakikutana mjini New York kwa mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu.

Akizindua chombo hicho akiwa ameandamana na nyota wa kandanda ambaye pia ni Balozi Mwema wa UNICEF, David Beckham, Ban amesema malengo ya maendeleo endelevu yanawaweka watu, katikati ya maendeleo, hususan watoto, akiongeza kuwa hatua ya kwanza ni kuyaridhia malengo hayo hapo kesho Septemba 25.

“Hatua ya pili ni kuwasikiliza watu ambao malengo haya yanalenga kunufaisha, hususan watoto na vijana. Ndiyo maana mradi wa “Baraza la Vijana” ni muhimu. Linawapa vijana chombo kipya cha kupazia sauti kinachowahusu, na mawazo yao kuhusu siku zijazo”

Akizungumza kuhusu ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu, Ban amedokeza kuhusu vipengele muhimu vya malengo hayo na dhamira ya kufikia maisha ya utu kwa wote.

Ameongeza kuwa kuweka maisha ya utu kwa wote kunamaanisha kutomwacha mtu yeyote nyuma.

“Kila mtu ni mshikadau katika malengo ya maendeleo endelevu, hususan vijana. Wataishi kesho katika dunia itakayotegemea hatua tunazochukua sasa”