Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laongeza mamlaka ya UNMIL hadi Septemba 30, 2016

Baraza la Usalama laongeza mamlaka ya UNMIL hadi Septemba 30, 2016

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja wamepitisha azimio la kuongeza muda wa mamlaka ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia, UNMIL, hadi Septemba 30, mwaka 2016.

Miongoni mwa mamlaka ya ujumbe huo, itakuwa ni ulinzi wa raia, kufanyia marekebisho taasisi za sheria na usalama, kuendeleza haki za binadamu na kuwalinda wahudumu wa Umoja wa Mataifa.

Aidha, azimio hilo limepunguza nguvu ya kijeshi ya UNMIL, kutoka askari jeshi 3,590 hadi askari jeshi 1,240, na polisi kutoka 1,515 hadi 606 ifikapo Juni 30, 2016.

Azimio hilo pia limesisitiza dhamira ya Baraza la Usalama kufanyia tathmini uwezo wa Liberia kujitosheleza kuhakikisha usalama na utulivu baada ya mpito wa usalama wa Juni 30, 2016 na hali ya usalama kwa ujumla nchini humo ifikapo Disemba 15, 2016, likitazamia kuundoa ujumbe huo wa UNMIL nchini Liberia.