Ban ataka rais wa Burkina Faso na Waziri Mkuu waachiliwe mara moja

Ban ataka rais wa Burkina Faso na Waziri Mkuu waachiliwe mara moja

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ameeleza kusikitishwa na kutekwa na kuzuiliwa kwa Rais Michel Kafando na Waziri Mkuu, Yacouba Isaac Zida wa Burkina Faso, pamoja na mawaziri kadhaa wa kitaifa, ambako kumefanywa na Régiment de Sécurité Présidentielle leo mjini Ouagadougou.

Taarifa ya msemaji wake imesema, Katibu Mkuu ametoa wito waachiliwe mara moja viongozi hao, akikitaja kitendo cha kukamatwa kwao kama ukiukaji wa Katiba ya Burkina Faso na Mkataba wa Mpito.

Ban amesema Umoja wa Mataifa unaunga mkono Rais Kafando kwa dhati.

Aidha, Bwana Ban amenukuliwa akisema kuwa anafahamu uungaji mkono wa dhati wawatu wa Burkina Faso kwa kipindi cha mpito cha amani, na kutoa wito ratiba ya mpito iheshimiwe, ukiwemo uchaguzi ujao.

Taarifa ya msemaji wake imeongeza kuwa, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Afrika Magharibi, Mohamed Ibn Chambas, yupo mjini Ouagadougou, na anashirikiana kwa karibu na Jumuiya ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS na Muungano wa Afrika, AU na wadau wengine wa kimataifa ili kutunza mamlaka ya mpito Burkina Faso.