Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani kuzuiliwa kwa Rais wa Burkina Faso, Waziri Mkuu na mawaziri wengine

Baraza la Usalama lalaani kuzuiliwa kwa Rais wa Burkina Faso, Waziri Mkuu na mawaziri wengine

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Jumatano jioni limelaani vikali kukamatwa na kuzuiliwa kwa Rais Michel Kafando na Waziri Mkuu, Isaac Zida wa Burkina Faso, pamoja na mawaziri kadhaa, likitaka waachiliwe wakiwa salama mara moja.

Katika taarifa, wajumbe wa Baraza la Usalama wamesisitiza kuwa kuzuiliwa kwa viongozi hao na mawakala wa Régiment de sécurité présidentielle ni ukiukaji wa katiba na mkataba wa mpito wa Burkina Faso.

Aidha, wajumbe hao wametoa wito kwa wahusika wote wa Burkina Faso wakujizuia na vitendo vyovyote vya ghasia.

Halikadhalika, wajumbe wa Baraza la Usalama wameelezea uungaji mkono wao thabiti kwa mamlaka za mpito za Burkina Faso, na kuwataka wahusika wote kuheshimu ratiba ya mpito, hususan kufanyika kwa uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika, ambao umepangwa kufanywa mnamo Oktoba 11 2015.