Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mateso ya walio wachache Mashariki ya Kati sasa ni mateso ya walio wengi: Eliasson

Mateso ya walio wachache Mashariki ya Kati sasa ni mateso ya walio wengi: Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatma ya makundi ya walio wachache kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati, huku wakiendelea kuteswa na vikundi vya waasi wenye itikadi kali ya kidini.

Bwana Eliasson amesema hayo akiongea na Redio ya Umoja wa Mataifa baada ya kuhudhuria mkutano kuhusu mateso dhidi ya jamii za kidini uliofanyika jumanne hii mjini Paris Ufaransa.

Idadi ya watu kutoka makundi ya walio wachache imepungua sana tangu kipindi cha miaka kumi iliyopita. Ukiangalia wakristo, walikuwa takriban milioni 2 miaka kumi iliyopita, sasa wako 500,000. Kwa hiyo ni mwelekeo mbaya wa muda mrefu ambao unaenda kinyume na mchanganyiko wa watu ambao ulikuwepo mashariki ya kati zamani.”

Amesema siyo wakristo tu ambao wanateswa bali pia jamii nyingine akiongeza kwamba sasa ni walio wengi ambao wanateswa na kundi la waasi wa ISIS nchini Iraq na Syria.

Hatimaye Bwana Eliasson amesema suluhu si tu ya kijeshi bali pia mabadiliko ya jamii nzima yanahitajika na kuwapatia vijana matumaini mapya kwa mustakhabali wao. Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unatarajia kuzindua mpango kazi wa kupambana na hatari za ugaidi mwezi Novemba mwaka huu.