Kiribati yapitisha sheria ya kuwalinda watoto wanaokabiliwa kisheria

Kiribati yapitisha sheria ya kuwalinda watoto wanaokabiliwa kisheria

Shirika la Kuwahudumia Watoto, UNICEF, limekaribisha leo hatua ya taifa la Kiribati [KIRIBASI] ya kupitisha sheria kuhusu mfumo wa sheria ya watoto, ambayo itahakikisha kuwa watoto wote na vijana wanaoshtakiwa au kudaiwa kufanya kosa lolote wanashughulikiwa kwa heshima na kulindwa. Taarifa kamili na Joseph Msami

Taarifa ya Msami

Kwa sasa nchini Kiribati, kuna watoto 10 wanaozuiliwa katika jela za watoto. UNICEF imesema watoto hao na barubaru, pamoja na wengine waliowatangulia, walilazimika kukabiliana na mfumo wa sheria unaoshughulikia masuala ya watu wazima, wakizuiliwa na watu wazima na pia kushtakiwa kama watu wazima.

Sheria hiyo ambayo imesifiwa na UNICEF kama inayowajali watoto, itaweka viwango wastani vya mfumo wa sheria ya vijana, ikijikita hasa katika kuwatenganisha watoto na jela za watu wazima.

Sheria hiyo pia inatoa fursa kwa jamii kushiriki katika kurekebisha tabia ya watoto na kuwarejesha tena katika jamii, na hivyo kuhakikisha mila na tamaduni za Kiribati zinajumuishwa katika mfumo wa sheria wa vijana inapowezekana.