Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhasimu kati ya serikali na NGOs haufai kuelekea SDGs: Ban

Uhasimu kati ya serikali na NGOs haufai kuelekea SDGs: Ban

Mkutano wa Nne wa maspika wa mabunge duniani umeanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, ambapo Katibu Mkuu Ban Ki-moon ametaka serikali na mashirika ya kiraia kuwa wadau na si mahasimu katika kusimamia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDG. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kauli mbiu ya mkutano huo wa siku tatu ni demokrasia kwa amani na maendeleo endelevu na kujenga dunia itakakiwayo ambapo akizungumza kwenye ufunguzi Katibu Mkuu Ban amesema mwelekeo sasa ni kuhakikisha malengo 17 ya SDG yanafanikiwa kupitia ushirikiano baina ya serikali, umma na raia. Hata hivyo amesema kuna changamoto kwa kuwa..

(Sauti ya Ban)

“Serikali kadhaa zimeridhia mbinu zinazokwamisha mashirika ya kiraia kufanya kazi zao au kuweka ukomo wa fedha wanazoweza kupokea au mambo yote mawili. Tunavyoelekea kwenye ajenda mpya, serikali na mashirika ya kiraia wanapaswa kuwa wadau katika kujenga mustakhbali tunaoutaka.”

Awali Rais wa IPU Saber Chowdhury akatanabaisha..

(Sauti ya Saber)

“Tunakutana hapa kuhakikisha kuwa ambazo zilizotolewa na serikali zetu zinazingatiwa. Na ndio maana mkutano huu ni tofauti na mikutano mingine inayofanyika.”

Mkutano huo hufanyika kila baada ya miaka mitano na umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya IPU na Umoja wa Mataifa.