Skip to main content

UNEP yazindua kifaa kinachoweza kupunguza vifo vitokanavyo na uchafuzi wa hewa

UNEP yazindua kifaa kinachoweza kupunguza vifo vitokanavyo na uchafuzi wa hewa

Shirika la Mpango wa Mazingira, UNEP, imezindua leo kifaa kupima ubora wa hewa mjini Nairobi, ambacho kinatarajiwa kusaidia kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na uchafuzi wa hewa nje. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Kifaa hicho kinataraijwa kugharimu mara mia chini ya gharama ya vifaa vilivyopo sasa, na kinatarajiwa kubadili kwa kiasi kikubwa jinsi ubora wa hewa unavyopimwa katika nchi zinazoendelea.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNEP, kifaa hicho chenye uwezo wa kukusanya vigezo vyote muhimu vya ubora wa hewa, kitagharimu takriban dola 1,500 kila kimoja, na hivyo kuziwezesha serikali kuweka mtandao wa kitaifa wa vifaa kama hivyo kwa gharama ya kati ya dola 150,000 na 200,000 pekee. Kwa sasa, kiasi hicho cha fedha kinahitajika kuweka kifaa kimoja tu cha aina zinazotumika sasa.

Wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Achim Steiner amesema uchafuzi wa hewa husababisha vifo milioni 7 vya mapema duniani kila mwaka, huku uchafuzi wa hewa nje ya nyumba ukichangia nusu ya idadi hiyo ya vifo, ambavyo amesema vinaweza kuzuiliwa.