Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yakaribisha tangazo la Uingereza na Ufaransa kuhusu suala la Calais

UNHCR yakaribisha tangazo la Uingereza na Ufaransa kuhusu suala la Calais

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, António Guterres, amekaribisha tangazo la leo la Ufaransa na Uingereza kuhusu hali ya wakimbizi na wahamiaji katika mji wa Calais, Ufaransa, na hatua zilizopangwa kuchukuliwa kulipatia suluhu.Taarifa Kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Bwana Guterres amesema anashukuru kwamba serikali hizo mbili zimechukua mtazamo wa pamoja ili kukabiliana na suala kanganishi la Calais, akikaribisha hasa vipengele vya kibinadamu na ulinzi vya mpango huo.

Wakati huo huo, ametambua umuhimu wa kupambana na ulanguzi na usafirishaji haramu, ambao huwanyanyasa watu walio hatarini. Kwa mantiki hiyo, amesema ni muhimu kutambua kuwa, ili kufaulu kukabiliana na walanguzi na wasafirishaji haramu wa binadamu, ni lazima ziongezwe njia za kisheria za kuwawezesha watu wanaotafuta hifadhi kwenda Ulaya.

Amesema wengi wa watu walioko Calais huenda wanahitaji ulinzi wa kimataifa, wakiwa wametoka nchi zenye migogoro, mathalan Afghanistan, Eritrea, Somalia, Sudan na Syria.