Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP kupunguza kwa nusu chakula cha wakimbizi Iraq

WFP kupunguza kwa nusu chakula cha wakimbizi Iraq

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula, WFP limetangaza leo kulazimika kupunguza kiasi cha chakula kinachopatiwa kwa wakimbizi wa ndani milioni moja waliopo nchini Iraq.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, WFP imesema ukosefu wa ufadhili na ongezeko la idadi ya wakimbizi wa ndani imewalazimu kupunguza kwa nusu chakula kwa wakimbizi wanaoishi nje ya kambi. Vifurushi vya chakula vitatimiza asilimia 40 tu za mahitaji ya familia kwa mwezi, ikilinganishwa na asilimia 80 awali.

Nelly Opiyo ni ofisa wa WFP nchini Iraq.

"Tumehoji karibu familia 16,000 kwenye eneo hilo la Kurdistan nchini Iraq, na tumepata familia 4,615 ambazo tayari zimekuwa na uwezo wa kujitegemea. Wale ambao watakuwa na uwezo wa kutimiza mahitaji yao ya chakula, tutawapa msaada sawa na dola 10 kwa kila mtu kwa mwezi, huku wale ambao bado wanateseka tutaendelea kuwapa dola 19 kwa kila mtu kwa mwezi. »

WFP inakadiria kuwa raia wa Iraq milioni tatu wamekimba makwao tangu mwanzo wa mapigano , WFP ikifikisha msaada wa chakula kwa wakimbizi wa ndani milioni 1.8.