Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata wasababisha WFP kupunguza misaada kwa wakimbizi wa Syria

Ukata wasababisha WFP kupunguza misaada kwa wakimbizi wa Syria

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limetangaza leo kulazimika kupunguza misaada ya chakula kwa wakimbizi wa Syria waliopo nchini Lebanon na Jordan kwa sababu ya uhaba wa fedha.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, WFP imesema kwamba mwezi huu wa Julai itapunguza kwa nusu thamani ya vocha za chakula wanazopatiwa wakimbizi nchini Lebanon, ambapo sasa kila mtu atapatiwa vocha ya dola 13 na Nusu kwa mwezi.

Hata hivyo WFP imeonya kuwa mwezi wa Agosti huenda ikalazimika kusitisha kabisa misaada inayowapa wakimbizi zaidi ya 400,000 wasioishi kambini, iwapo haitapata fedha.

WFP inahitaji hivi sasa dola milioni 139 ili kuendelea kusaidia wakimbizi waliopo Jordan, Lebanon, Misri, Uturuki na Iraq hadi mwezi Septemba.