Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Mapema Ijumaa, KM BanKi-moon alikutana mjini Stockholm na Spika wa Bunge pamoja na wawakilishi wa vyama vya kisiasa. Baada ya hapo KM alikuwa na mazungumzo na wawakilishi wa mashirika yasio ya kiserikali ya Uswidini. Kufuatia hapo KM alielekea Copenhagen, ambapo alitarajiwa kukutana kwa mazumgumzo na Waziri Mkuu wa Denmark, Lars Lokke Rasmussen, na vile vile Jacques Rogge, Raisi wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC). Ijumamosi KM atahutubia Baraza Kuu la Olimpiki ambapo aantazamiwa kujadilia ajenda ya Kamati ya IOC kuhusu Hifadhi ya Mazingira kwenye Shughuli za Michezo.

Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu linalokutana Geneva leo limepitisha maazimio sita kuhusu mada kadha: zikijumlisha mada zinazohusu uhuru wa kujieleza na uhuru wa maoni; ufyekaji wa ubaguzi dhidi ya wanawake; athari mbaya za utupaji wa kihorera wa taka za sumu dhidi ya haki za binadamu; athari za madeni ya kutoka nchi za kigeni katika maamirisho ya haki za binadamu; fungamano za umaskini uliovuka mipaka na haki za binadamu; Aung San Suu Kyi na wafungwa wengine wa kisiasa katika Myanmar; na utekelezaji wa haki za binadamu kwa uwiano na maadili ya ubinadamu na sheria ya kimataifa juu ya haki za binadamu.

Mashirika ya UM kadha hivi sasa yameripotiwa kushirikiana na Serikali ya Indonesia katika kuwasaidia kihali wakazi wa Sumatra ya Magharibi. Vile vile UM unasaidia kuratibu na jumuiya za kimataifa zinazohudumia misaada ya kiutu, mipango ya kufarajia umma ulioathirika na tetemeko la ardhi liliotokea karibuni Sumatra Magharibi. Timu ya UM ya Kuratibu na Kutathminia Maafa (UNDAC) ipo Indonesia kutayarisha juhudi za kimataifa za kutafuta na kuokoa waathirika walionaswa na miporomoko ya majengo kwenye mazingira ya zilzala. Vile vile UM umeshatuma kwenye eneo la maafa vifaa vya kusaidia familia, pamoja na kutuma mahema ya skuli za muda, na vifaa vyenginevyo vya kuhudumia uzazi, na pia kupeleka zile zana nzito za kusafisha vifushi. Kwa mujibu wa ripoti za UM juu ya Huduma za Dharura (OCHA) zilzala iliopiga Sumatra, Indonesia karibuni, yenye Kipimo cha Richter cha 7.6, imesababisha mamia ya vifo, watu 2,400 walijeruhiwa, maelfu ya raia walinaswa chini ya majengo yalioporomoka, na karibu nyumba 20,000 ziliharibiwa vibaya sana.

OCHA imeripoti dhoruba ya majira ya joto iliopiga majuzi katika Philippines, imeathiri vibaya maisha ya watu milioni 3.1 na kusababisha vifo 293, na watu 42 wametangazwa kupotea. OCHA imeeleza pia ya kuwa watu 651,000 wameshahamishwa kwenye vituo 508 vya makazi ya muda. Hata hivyo juhudi za kupeleka misaada ya kufarajia mahitaji ya kihali kwa waathirika zinaelezewa kupwaya kidogo kwa sasa, kwa kukhofia Kimbunga Parma ambacho kinaashiriwa kupiga Philippines katika mwisho wa wiki hii. OCHA ina wasiwasi juu ya taarifa hizo, kwa sababu watu milioni 8.5 wanakadiriwa kuishi kwenye mkondo utakaopitia kimbunga, hasa wale milioni 1.8 ambao wanaishi kwenye zile sehemu ambazo dhoruba inatarajiwa kupiga kwa nguvu zaidi.

Christine McNab wa Uswidin ameteuliwa na KM kuwa Naibu Mjumbe Maalumu mpya kwa Iraq. Anatazamiwa pia kushika madaraka ya mkuu wa kitengo kitakachohusika na Misaada ya Kiutu na Maendeleo kwenye Shirika la UM la Usaidizi wa Amani Iraq (UNAMI), na vile vile kushika wadhifa wa Mratibu Mkaazi wa UM kuhusu misaada ya kiutu. Atamrithi David Shearer, ambaye KM alimshukuru kwa mchango wake wa kuongoza, kwa mafanikio, ushirikiano bora kikazi miongoni mwa mashirika ya UM yaliopo Iraq. McNab ana uzoefu mkubwa kuhusu huduma za maendeleo, hasa katika utendaji wa mageuzi ya kwenye sekta za maendeleo, utawala wa kidemokrasia na katika kukuza uwezo wa kutekeleza, kwa wakati, Maendeleo ya Malengo ya Milenia (MDGs). Hivi sasa McNab ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) katika Bosnia na Herzegovina, na kabla ya hapo, mnamo 2002 mpaka 2006 McNab alishika wadhifa kama huo katika Jordan.

Naibu KM Asha-Rose Migiro asubuhi alihutubia kikao kisio rasmi cha Baraza Kuu na kusailia mada inayohusu utaratibu wa kuhisihimu na kufuata sheria. Alizungumzia pia kama ni Mwenyekiti wa Kundi la Uratibu wa Kutekeleza Ufuataji Sheria Kimataifa, ambapo alikumbusha ya kuwa UM imejihusisha katika nchi 120 kwenye shughuli za kuimarisha miradi ya ufuataji sheria. Alielezea namna Mradi wa Pamoja unavyotekelezwa katika kuongoza kazi za idara na mashirika makuu tisa ya UM yanayojishughulisha na kadhia hiyo ya kisheria. Alitumai Mradi wa Pamoja utasaidia kuimarisha mwambatano wa kazi, kuyahusisha Mataifa Wanachama kwa kuongeza nguvu za utendaji kimataifa kwa mintarafu ya kuhishimu na kufuata sheria kama inavyostahiki.

Wajumbe wapatanishi wanaohudhuria kikao cha matayarisho cha UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa katika mji wa Bangkok, Thailand wamekamilisha wiki ya kwanza ya vikao vya mwisho mwisho kabla ya kufanyika Mkutano Mkuu wa Copenhagen katika mwezi Disemba. Yvo de Boer, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya UM kuhusu Mkataba wa Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC) amenakiliwa akisema amefurahika kuona maendeleo yalipatikana kwenye maandalizi ya sehemu kadha muhimu za mswada wa mapatano ya kikao cha Copenhagen, hasa kwenye yale masuala yanayoambatana na marekibisho yanayofaa kukabiliana vyema na athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye nchi zinazoendelea, kwa kutumia teknolojiya mpya na kujenga uwezo unaotakiwa kuyadhibiti mabadiliko husika. Alisema pia kwamba aliingiwa moyo kuona wajumbe wa kimataifa walizingatia kwa makini zaidi waraka wa majadiliano, na walitoa vile vifungu ambavyo havina uhusiano juu ya udhibiti wa mabadiliko ya hali ya hewa.