Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya miaka 70, UM unaendelea kutimiza ndoto za waasisi: Ban

Baada ya miaka 70, UM unaendelea kutimiza ndoto za waasisi: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema wakati wa vita vikuu vya pili dunia watu walikataa tamaa, lakini matumaini yaliibuka tena wakati wa kuunda Umoja wa Mataifa mwaka 1945.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka sabini ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika leo mjini San Francisco, Marekani, ambapo mkataba wa Umoja wa Mataifa ulisainiwa na nchi 50, tarehe 26, Juni, mwaka 1945, Bwana Ban amesema waasisi walijenga Umoja huo wakiwa na maadili na ndoto za kuona dunia yenye amani.

“ Kuandika Mkataba wa Umoja wa Mataifa kulikuwa ni kitendo adhimu cha kubahatisha .Wawakilishi wa makumi ya nchi walibahatisha kuhusu ubinadamu. Imani zilipotea sana katika handaki na vyumba vya gesi za kuua vya vita mbili za dunia, katika kipindi cha kizazi kimoja tu, lakini wameweza kuamini kitu kikubwa zaidi kuliko watu au nchi.”

Amesimulia jinsi yeye mwenyewe alisaidiwa na Umoja wa Mataifa baada ya vita vya Korea, wakati ambapo kijiji chake na shule yake viliteketezwa, akisema Umoja wa Mataifa uliwaonyesha kwamba hawakutelekezwa.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson ameeleza umuhimu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa, akisema mwenyewe anaibeba kila siku mfukoni ili kukumbuka kwamba Umoja huo umejengwa juu ya maadili na masharti, na kuongeza kwamba jamii ya kimataifa inawajibika kutimiza matumaini ya waanzilishi wake, yaani kuepuka na vita, kulinda haki za binadamu na kutokomeza umaskini.