Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukraine: hali ya kibinadamu yazidi kuwa tete mashariki mwa nchi

Ukraine: hali ya kibinadamu yazidi kuwa tete mashariki mwa nchi

Kati ya Aprili katikati na tarehe 3 Juni mwaka huu, idadi ya wakimbizi wa ndani imefika zaidi ya milioni 1.3 nchini Ukraine, hasa kwenye majimbo ya mashariki ya Donetsk, Luhansk and Kharkivska, amesema msemaji wa Shirka la Umoja wa Mataifa la Kuratibu misaada ya kibindamu OCHA, Jens Laerke, akitaja takwimu za Wizara ya Maswala ya Kijamii ya Ukraine.

Bwana Laerke amewaambia waandishi wa habari leo mjini Geneva kwamba wakati huo huo watu wapatao 6,454 wameuawa, huku wengine 16,146 wakijeruhiwa, na idadi ya waliotafuta hifadhi kwenye nchi jirani imefika 878,000.

Ameongeza kwamba mapigano yanaendelea mashariki mwa nchi, watu wakilazimika kuhama makwao na wakikumbwa na hatari ya mabomu yaliyotegwa ardhini.

Aidha msemaji huyo amesema kwa ujumla ni watu milioni 5 wanaohitaji msaada wa kibinadamu, huku milioni 3.2 wakilengwa na Mpango wa Kuratibu misaada ya kibindamu unaotekelezwa na Umoja wa Mataifa, lakini mpango huo wa dola milioni 316 umefadhiliwa kwa asilimia 24 tu.

Hatimaye ameeleza kwamba upatikanaji wa maji ni moja ya mahitaji makubwa kwenye maeneo ya mapigano.

Upatikanaji wa maji unazidi kuhitajika.  Kwenye kijiji cha Mariinka, ambapo mapigano yalitokea, tunakadiria kwamba watu 10,000 wamekosa huduma za maji kwa kipindi cha siku kadhaa zilizopita. Serikali za mitaa zinajaribu kuweka maji kwenye tanki kutoka vyanzo mbali mbali kwenye eneo hili, lakini haitoshi. Pia kwenye maeneo ya Luhansk yasiyotawaliwa na serikali, maelfu wameripotiwa kukosa kabisa huduma za maji.”