Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maji si kwa ajili ya uhai tu, maji ni uhai: Ban Ki-moon

Maji si kwa ajili ya uhai tu, maji ni uhai: Ban Ki-moon

Maji ni afya, utu na haki ya binadamu, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akihutubia viongozi wa dunia kwenye kongamano la kimataifa kuhusu maji kwa uhai, ambalo linafanyika wiki hii mjini Dushanbe, nchini Tajikistan.

Bwana Ban amesema uelewa wa jamii ya kimataifa kuhusu masuala ya maji na kujisafi umeongezeka katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

“ Dunia imetimiza lengo la maendeleo ya milenia kuhusu maji safi na endelevu ya kunywa, miaka mitano kabla ya ukomo wa ratiba. Kwa kipinid cha kizazi kimoja, watu bilioni 2.3, theluthi moja ya wanadamu, wamepata vyanzo imara vya maji ya kunywa”

Ban amesema suala la maji linaathiri harakati za uwezeshaji wa wanawake

“Kote duniani, ukizingatia suala la maji, wanawake na wasichana ndio wanaobeba uzito zaidi. Mzigo wa kutafuta maji ya kunywa hubebwa zaidi na wanawake na wasichana, ambao hutumia saa milioni mia mbili kila siku wakitega maji. Uhaba wa vifaa vya kujisafi pia huathiri elimu na uzalishaji wa kiuchumi wa wanawake na wasichana, na pia utu na usalama wao binafsi.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema suala la maji linapaswa kuwekwa kipaumbele kwenye ajenda ya maendeleo endelevu itakayoamuliwa mwezi Septemba mwaka huu.