Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajali ya moto kiwandani Ufilipino ni ishara ya mazingira duni yakumbayo wafanyakazi:ILO

Ajali ya moto kiwandani Ufilipino ni ishara ya mazingira duni yakumbayo wafanyakazi:ILO

Ajali ya moto kwenye kiwanda cha viatu huko Ufilipino, ni kiashiria cha mazingira hatarishi ya kazi ambamo kwayo wafanyakazi wengi wanakumbana nayo.

Ni kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kazi duniani, ILO, Guy Rider katika salamu zake za rambirambi kwa familia za wafanyakazi zaidi ya 72 wanaoripitiwa kufariki dunia katika ajali ya moto ya Jumatano kwenye kiwanda hicho mjini Manila ulioteketeza kiwanda chote.

Amesema yuko pamoja na familia za wafiwa akisema kwa mara nyingine tena dunia inaomboleza vifo vya wafanyakazi ambao maisha yao yamekatishwa kutokana na ajali za kazini ambazo mara nyingine zinazuilika.

Bwana Rider amesema kila mtu ana haki ya kufanya kazi katika mazingira salama bila kujali mahali anakofanya kazi na kazi anayofanya.

Mkurugenzi mkuu huyo wa ILO amesema mazingira ya kazi yanaweza kuwa salama kwa kufanya ukaguzi mara kwa  mara kuhakikisha yanakidhi vigezo vya usalama vinavyotakiwa ikiwemo moto, majengo na umeme.

Amesema ILO kwa upande wake iko tayari kusaidia kwa kushirikiana na waajiri na vyama vya wafanyakazi na wadau wote kuhakikisha usalama pahala pa kazi.