Skip to main content

Mweleko Vanuatu baada ya Pam unatia moyo:OCHA

Mweleko Vanuatu baada ya Pam unatia moyo:OCHA

Miezi miwili tangu kimbunga Pam kipige visiwa vya Vanuatu, hali ya kujikwamua kutokana na madhara ya kimbunga hicho inatia moyo ambapo wananchi wamenufaika na usaidizi unaotolewa na serikali kwa ushirika na wahisani.

Mratibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu, OCHA nchini Vanuatu Osnat Lubrani amesema mathalani zaidi ya watu 21,000 wamepokea misaada kama vile maji safi na salama ilhali zaidi ya 26,000 wamenufaika na usaidizi wa ukarabati wa mifumo ya maji.

Hata hivyo Lubrani amesema bado usaidizi zaidi unahitajika kwani ombi la fedha za usaidizi kwa Vanuatu limechangiwa kwa asilimia 59 tu huku mahitaji yakiwa bado makubwa.

Kimbunga Pam kilipiga tarehe 13 Machi na kuharibu makazi na njia za watu kujipatia vipato katika majimbo Sita ya nchi hiyo.