Mkuu wa MINUSMA alaani mashambulizi dhidi ya jeshi la Mali

Mkuu wa MINUSMA alaani mashambulizi dhidi ya jeshi la Mali

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Mali, na mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSMA, Hamdi Mongi, amelaani vikali mashambulizi yaliyotokea asubuhi hii dhidi ya jeshi la taifa la Mali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na MINUSMA, waasi kutoka kundi la kuratibu jumuiya za Azawad (CMA) wameshambulia askari wa jeshi la serikali wakati wakiwa doria kwenye barabara ya kutoka Timbukutu hadi Goundam.

Bwana Mongi amesema tukio hilo ni ukiukaji wa makubaliano ya sitisho la mapigano ya Mei, 2014, akiongeza kwamba ghasia zinapaswa kusitishwa mara moja.

Amezisihi pande zote kuonyesha ziko tayari kusaini makubaliano ya amani tarehe 15 mwezi huu jinsi ilivyopangwa awali, akizingatia kwamba ni wananchi wa Mali wenyewe tu wataweza kufikia amani ya kudumu nchini humo.