Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kobler ashawishi waasi wa FDLR kurudi Rwanda.

Kobler ashawishi waasi wa FDLR kurudi Rwanda.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini DRC, Martin Kobler, amewashawishi waasi wa FDLR waliojisalimisha kukubali kurudi Rwanda, kupitia mfumo maalum wa kuwarejeshea makwao na kuwasaidia kuungana tena na jamii, DDRRR.

Bwana Kobler ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO amesema hayo alipotembelea kambi ya Jenerali Bahuma kwenye eneo la Kisangani nchini DRC ambako tayari waasi 807 wa FDLR walijisalimisha pamoja na familia zao.

Kwa mujibu wa taarifa ya MONUSCO, Bwana Kobler amekuwa na maongezi ya moja kwa moja na baadhi wa waasi hawa ili kuwaondoa hofu ya kuchukua uamuzi wa kurudi Rwanda, akisikitishwa kwamba baadhi ya maofisa waliopo kambini wanawazuia wengine kurudi kwao.

Aidha MONSUCO imesema tani saba za vyakula zitasafirishwa kwa ajili ya mahitaji yao kambini.

Bwana Kobler amesema tayari MONUSCO imewarejesha nchini Rwanda waasi wa FDLR 12,000 tangu 2001.