Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya Ebola, Liberia yaanza tena chanjo dhidi ya Polio na Surua

Baada ya Ebola, Liberia yaanza tena chanjo dhidi ya Polio na Surua

Kampeni ya wiki moja ya kuwapatia watoto zaidi ya Laki Sita chanjo dhidi ya Polio na Surua imeanza nchini Liberia ikiongozwa na Wizara ya afya kaw ushirikiano na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kuhudumia watoto UNICEF na lile la afya WHO na kituo cha udhibiti magonjwa, CDC.

Awali kampeni hiyo ya aina yake iliwakuwa ifanyike mwaka jana lakini ilisitishwa kutokana na mlipuko wa Ebola ambapo Liberia inasema mkwamo huo umeweka hatarini watoto wengi kukumbwa na magonjwa hayo.

Chanjo dhidi ya Polio italenga watoto weney umri wa chini ya miaka mitano ilhali ile ya Surua ni kwa watoto wa kuanzia miezi Sita hadi chini ya miaka mitano.

Christopher Boulierac ni msemaji wa UNICEF.

(Sauti ya Boulierac)

“Kampeni kubwa ya kuhamasisha umma imeanza ili kushawishi umma juu ya umuhimu watoto wao kupatiwa chanjo katika mtazamo mgumu wa sasa, na kuelezea hatua zinazochukuliwa kupunguza hatari yoyote ya maambukizi.”

Mlipuko wa Ebola uliathiri mifumo yote ya afya ikiwemo utoaji wa chanjo, mathalani utoaji wa chanjo dhidi ya Surua uliporomoka kwa asilimia 45 kati ya Agosti na Disemba 2014 kwa mujibu wa serikali ya Liberia.