Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi kubwa ya wakimbizi wa Burundi wawasili Rwanda :UNHCR

Idadi kubwa ya wakimbizi wa Burundi wawasili Rwanda :UNHCR

Mwishoni mwa wiki idadi ya wakimbizi wa Burundi wanaovuka mpaka na kuingia nchini Rwanda imeongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia zaidi ya wakimbizi 5000 waliovuka katika siku mbili pekee.

Kwa mujibu wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa mataifa UNHCR, serikali ya Rwanda imesema tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa April raia wa Burundi 21,000 wamekimbilia Rwanda kutokana na vitisho vinavyohusiana na ghasia za kabla ya uchaguzi.

Serikali ya Rwanda imetenga eneo maalumu mjini Mahama kwenye jimbo la Mashariki ili kufungua kambi mpya ya wakimbizi. UNHCR na washirika wake wanahamisha wakimbizi kuwapeleka kwenye kambi hiii mpya kila siku, wakiwa na msafara wa watu 1,500.

Rwanda tayari inahifadhi wakimbizi Zaidi ya 74,000 wengi kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Saber Azam ambaye ni mwakilishi wa UNHCR nchini Rwanda anaeleza wanachowaambia wakimbizi hao.

« Hasa wanataja tishio la usalama kutoka kwa kundi la vijana linaloitwa Imbonerakure, ambao naamini ni wafuasi wa upande moja. Hadi sasa hakuna dalili ya kulenga jamii moja pekee, wakimbikizi hao wanatoka maeneo ya mpakani, na wengi wao ni wanawake na watoto »