Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa unasisitiza umuhimu wa uchaguzi katika utaratibu wa mpito nchini CAR

Umoja wa Mataifa unasisitiza umuhimu wa uchaguzi katika utaratibu wa mpito nchini CAR

Mkuu wa idara ya ulinzi wa amani ya Umoja wa Mataifa Hervé Ladsous amefurahia dalili za kurejelea kwa hali ya usalama na shughuli za kiuchumi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana leo na rais wa mpito wa CAR, Catherine Samba-Panza, katika ziara yake ya siku nne nchini humo.

Amesema wiki hii ni muhimu kwani kongamano la maridhiano la Bangui linatarajia kuanza, aidha baraza la usalama linatakiwa kuongeza mamlaka ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Car, MINUSCA, kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kuhusu uchaguzi, amesema hatua hiyo ni ya msingi katika utaratibu wa mpito.

“ Kwa sasa kipaumbele zaidi ni kufanyika kwa uchaguzi huu muhimu katika muda uliopangwa na kwenye mazingira tulivu. Uchaguzi huu utawezesha kutoka katika kipindi cha mpito na kuunda serikali itokanayo na chaguo la kidemokrasia la wapiga kura”

Halikadhalika bwana Ladsous ametembelea maeneo ya kaskazini ya nchi ambapo bado mapigano yanaendelea.