Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wayemen wenyewe ndio watafanikisha mustakhbali wao: Benomar

Wayemen wenyewe ndio watafanikisha mustakhbali wao: Benomar

Suluhu la mzozo wa Yemen ni lazima litokane na mashauriano yanayoongozwa na wananchi wenyewe.

Ni sehemu ya ujumbe uliowasilishwa mbele ya baraza la Usalama na Jamal Benomar, ambaye ni mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen anayemaliza muda wake baada ya kujiuzulu.

Akiwapatia muhtasari waandishi wa habari wa lake yaliyojiri kwenye kikao hicho cha faragha, Benomar amesema licha ya kwamba kunaonekana kuna changamoto lakini hatua kama vile mkutano wa maridhiano ya kitaifa uliohitimishwa kwa mafanikio makubwa mwaka 2014 zimeweka misingi ya kuchagiza upya mpito wa kisiasa ali mradi pande zote zinashiriki.

(Sauti ya Benomar)

“Nimesisitiza kuwa kurejesha mchakato wa kisiasa na kupata amani na utulivu wa kudumu nchini Yemen kunawezekana pale tu mchakato huo ukiongozwa na wayemen wenyewe ambapo wataamua mustakhbali wao bila kuingiliwa au shinikizo za kigeni.”

Katika kikao hicho Benomar amekumbusha baraza kuwa azimio lake namba 2216 la mwaka huu kuhusu Yemen bado halijatekelezwa na kikundi cha Al Qaeda kwenye rasi ya Arabuni kinazidi kujinufaisha na mzozo unaoendelea nchini humo.