Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 29 baada ya janga la Chernobyl, Umoja wa Mataifa waendelea kukumbuka waathirika

Miaka 29 baada ya janga la Chernobyl, Umoja wa Mataifa waendelea kukumbuka waathirika

Leo tarehe 26 ikiwa ni miaka 29 baada ya ajali ya kinyuklia ya Chernobyl, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anawakumbuka mamia ya wafanyakazi waliojitolea kutoa usaidizi kwa dharura na watu zaidi ya 330,000 waliolazimika kuhama makwao baada ya janga hili.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Ban amenukuliwa akisema kwamba jamii ya kimataifa inaendelea kuwa karibu na mamilioni ya watu walioathirika na matokeo ya ajali hii katika maeneo ya Ukraine, Urusi na Belarus. Licha ya hayo, amefuraishwa na kuona kwamba raia kwenye maeneo hayo wameanza kuendelea na maisha ya kawaida.

Ameongeza kwamba Umoja wa Mataifa umetengeneza mpango wa kuisaidia jamii ya Chernobyl, kukuza maendeleo, maisha yenye afya na kujitegemea kwa jamii.

Wakati muongo wa Uponaji na Maendeleo endelevu kwa Chernobyl ukifikia ukomo mwaka 2016, Katibu Mkuu ameomba mkakati endelevu upatikane ili kutimiza uponaji wa eneo hilo na kushirikiana kwa ajili ya usalama wa nyuklia duniani kote.