Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IMO yakaribisha mpango wa Muungano wa Ulaya kuhusu zahma za Mediteranian

IMO yakaribisha mpango wa Muungano wa Ulaya kuhusu zahma za Mediteranian

Katibu Mkuu wa shirika la kimataifa la masuala ya majini IMO amekaribisha mpango wa Muungano wa Ulaya wa vipengee 10 kabla ya kikao maalumu cha baraza la Ulaya kitakachofanyika Alhamisi kushughulikia hali inayoendelea katika bahari ya Mediteranian.

Katibu Mkuu huyo  Koji Sekimizu amekaribisha mpango wa kutaka kuchukua hatua za haraka ili kukabiliana na vifo vya wahamiaji , mpango uliopitishwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Muungano wa Ulaya.

Bwana Sekimizu amesema kwa maoni yake mpango huo unawasilisha hatua za lengo la awali la kuzuia boti zilizofurika kufanya safari zisizosalama katika bahari ya Mediteraniani.

Amesema hatari sio tuu kwa wahamiaji wanaosafili na meli hizo zisizosalama bali pia ni kwa askari jasiri wanamaji na walinzi katika Pwani ya Mediteranian ,pia wakiwemo wavuvi ambao wako msitari wa mbele kuwatafuta na kuwaokoa wahamiaji wanaozama.

Ameongeza kuwa hatua zinahitajika kuchukuliwa dhidi ya wahalifu ambao wanakusanya wasafiri bila mpango na kuwarundika kupita kiasi katika meli zisizosalama, lakini pia kuna haja ya kuwa na hatua ya kuratibu uingiaji wa wahamiaji ili wasinyonywe na kunyanyasika .