Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na ING waendeleza ubia kuboresha maisha ya barubaru duniani

UNICEF na ING waendeleza ubia kuboresha maisha ya barubaru duniani

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na shirika moja la huduma za benki na kifedha nchini Uholanzi, ING wametangaza awamu ya pili ya ubia kati yao wenye lengo la kuboresha maisha ya vijana barubaru.

Awamu hiyo ya pili inafuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye awamu ya kwanza ya ushirikiano wao iliyolenga kuboresha elimu kwa watoto wanaoishi maeneo yasiyo rahisi zaidi kufikika huko Zambia, Ethiopia, India, Nepal na Brazil ambapo watoto zaidi ya Milioni Moja walinufaika.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Anthony Lake amekaribisha kuendelea kwa awamu hiyo ya pili kwa miaka mitatu ijayo ambapo ING inashawishi wafanyakazi na wateja wake kuchangia ili kubadilisha maisha ya watoto na barubaru.

UNICEF inasema zaidi ya vijana barubaru Bilioni Moja bado hawana huduma stahili za kuwawezesha kujitambua na kuwa na stadi za kuboresha maisha yao na jamii zao.

Kwa mantiki hiyo vijana barubaru 335,000 kutoka Kosovo, Montenegro, Nepal, Ufilipino na Zambia watanufaika na mpango huo ambapo Koos Timmermans Makamu Rais wa ING amesema wanaunga mkono harakati za UNICEF za kuboresha maisha na ustawi wa watoto na vijana duniani kote.