Skip to main content

Vurugu mashariki mwa DRC yahusiana na uhalifu wa kimataifa

Vurugu mashariki mwa DRC yahusiana na uhalifu wa kimataifa

Biashara haramu na uhalifu vinaendelea kukuza vurugu mashariki mwa Jamhuru ya Kidemokrasia ya Congo DRC, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP) na wadau wake.

Ripoti iliyotolewa leo inasema kwamba serikali ya DRC, licha ya kukabiliana na vurugu za kisiasa, pia inakumbwa na uhalifu unaofanywa na vikundi vilivyojihami vyenye ushirikiano na vikundi vya uhalifu vya kimataifa katika shughuli za magendo na utakasaji fedha.

Kwa mujibu wa ripoti hii, dhahabu, mbao, mkaa na rasimali pori kama vile pembe za ndovu vinauzwa kimagendo kwa thamani ya kati ya dola bilioni 0.7 na 1.3 kila mwaka, asilimia 98 za ujangili wa rasilimali pori zikivifikia vikundi vya uhalifu vya kimataifa, na asilimia 2 tu zikifaidi vikundi vilivyojihami mashariki mwa DRC na kuwapatia riziki takriban waasi 8,000.

Achim Steiner, mkurugenzi mtendaji wa UNEP amesema uhalifu huo unaipokonya nchi hiyo mapato ambavyo yangeweza kutumika kwa maendeleo endelevu na kutokomeza umaskini.

Naye mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, Martin Kobler, amesema mamia hayo ya dola yangeweza kutumiwa kulipa madaktari, walimu na kuendeleza uchumi.

Wataalam wamependekeza MONUSCO iimarishe mfumo wake wa kukusanya takwimu ili kutokomeza shughuli za uhalifu za vikundi vilivyojihami.