Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfuko wa kukwamua watoto dhidi ya utapiamlo waanzishwa:

Mfuko wa kukwamua watoto dhidi ya utapiamlo waanzishwa:

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto limezindua mfuko mpya wa kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia mamilioni ya watoto kwenye nchi maskini zaidi duniani kuondokana na utapiamlo na hivyo kufikia ukuaji wa kiafya unaoakiwa.

Uzinduzi huo umefanyika Washington, DC kando mwa vikao vya Benki ya Dunia ambapo UNICEF imesema kupitia mfuko huo uliopatiwa jina la Uthabiti wa lishe au The Power of Nutrition, nchi nufaika zitaweza kuanzisha au kuimarisha programu zao za lishe ili hatimaye kujenga jamii zenye afya na ustawi.

UNICEF inasema ushahidi unaonyesha kuwa lishe bora utotoni ni msingi wa ukuaji bora kimwili na kiakili na hivyo ni uwekezaji wenye manufaa makubwa.

Mfuko huo unaoweka dhahiri ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi unaungwa mkono na wadau mbali mbali wakiwemo wahisani binafsi, mashirika ya kimataifa ya maendeleo na lengo ni kufikia dola Bilioni Moja.

Dola Milioni 200 za awali zinatoka kwa wadau kama vile Benki ya dunia, Idara ya maendeleo ya kimatifa ya Uingereza na taasisi ya mfuko wa uwekezaji kwa watoto .