Roboti zinazoua zawatia wasiwasi watalaam wa Umoja wa Mataifa

Roboti zinazoua zawatia wasiwasi watalaam wa Umoja wa Mataifa

Uwajibikaji wa kimaadili kwenye matumizi ya roboti zinazoua zenyewe bila usimamizi wa binadamu ni mada ya mkutano ulioanza Jumatatu katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi.

Roboti hizo ambazo zina mifumo inayojitegemea ambayo inaziwezesha kuua bila usimamizi wa binadamu, au LAWS kwa kiingereza bado hazijaanza kutumiwa lakini watalaam wa Umoja wa Mataifa wanaamini kwamba sasa wakati umefika wa kujadili kuhusu matumizi yake.

Mwakilishi wa Kudumu wa Ujerumani kwenye mkutano wa kutokomeza silaha duniani huko Geneva, Uswisi, Michael Biontino amesema ni lazima kutambua uwajibikaji wa kimaadili kwenye matumizi ya silaha hizo ambazo zitaweza kuua mtu bila binadamu yeyote kuchukua uamuzi.

“ Mifumo hiyo ya kiotomatiki inayoua, LAWS itakuwa na matokeo gani kwenye utulivu wa ukanda na wa kimkakati? utaleta utulivu ama vurugu? Ni mwelekeo gani unaoweza kutarajiwa katika kusambaza mifumo ya kujitegemea ya kuua na silaha? Tunapaswa kujadili hayo”

Hata hivyo Balozi Biontino anaamini kuwa mkutano huo wa wiki moja unaweza kusaidia kuibua masuala ya kisheria, kimaadili, usalama na uwazi yanayotokana na teknolojia hiyo na hatimaye kufikia uamuzi wa kuzipiga marufuku kama vile nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa walivyoamua kuhusu silaha za zinazoondoa uwezo wa kuona mwaka 1995.