Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani mashambulizi ya Boko Haram

Baraza la Usalama lalaani mashambulizi ya Boko Haram

Wanachama wa Baraza la Usalama wamelaani vikali mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na kundi la Boko Haram kaskazini mwa Nigeria na Chad, yakiwemo yale ya Kwajafa, kwenye Jimbo la Borno, tarehe Tano Aprili, na ya Tchoukou Telia, tarehe Tatu Aprili.

Kupitia taarifa yao, wamepeleka salamu zao za rambirambi kwa familia za wahanga wakiwapa pole pia waliojeruhiwa, raia na serikali za Chad na Nigeria.

Aidha wanachama wa Baraza la Usalama wamezikumbusha nchi wanachama kwamba zinapaswa kuhakikisha hatua zilizochukuliwa kupambana na ugaidi zinaheshimu sheria ya kimataifa hasa haki za binadamu.

Hatimaye wameyasihi mashirika ya kiuchumi ya ukanda wa Afrika Magharibi na Afrika ya Kati, ambayo yanatarajia kukutana hivi karibuni kwenye kongamano la pamoja, kuunda mkakati wa pamoja na kushirikiana zaidi ili kupambana na Boko Haram, wakisisitiza kwamba kundi hilo ni tishio kwa ukanda mzima.