Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kushiriki kwenye kumbukizi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kushiriki kwenye kumbukizi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda

Mkuu wa Mfumo wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, MICT, John Hocking, Jumanne jioni atahudhuria kumbukizi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda itakayofanyika mjini Arusha na jamii ya wanyarwanda waliopo Tanzania.

Katika taarifa iliyotolewa wakati wa kukumbuka mauaji ya kimbari, MICT imesema kumbukizi maalum itafanyika pia jijini Dar es Salaam, kesho tarehe 8, Aprili, ikiwa ni pamoja na kusikiliza hotuba za viongozi wa Umoja wa Mataifa na Kamisheni Kuu ya Rwanda, kuwasha mishumaa na kuzindua maonyesho.

Kwa mujibu wa MICT, tangu kuundwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu kuhusu Rwanda, ICTR, tarehe 8, Novemba, mwaka 1994, watu 93 wameshtakiwa kwa msingi wa kuwajibika katika mauaji ya kimbari ya 1994, wakiwemo viongozi wa kisiasa, kijeshi na kidini.

MICT imeongeza kwamba wote walioshukiwa wamehukumiwa, isipokuwa watu 9.

MICT imeanzishwa mwaka 2010 na Baraza la Usalama na kupewa jukumu la kukamilisha kazi za ICTR zikiwa ni kusaka washukiwa waliobaki, kulinda usalama wa mashahidi na kuhitimisha adhabu za vifungo kwa waliohukumiwa.