Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wapunguzwa DRC, waongezwa CAR

Walinda amani wapunguzwa DRC, waongezwa CAR

Baraza la Usalama leo kwa kauli moja limepitisha azimio la kuongeza muda wa mamlaka za Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kwa mwaka mmoja zaidi. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Azimio la kuongeza muda huo pia limepunguza askari 2,000 kutoka kundi la walinda amani nchini DRC, ikiwa ni hatua ya kwanza ya mkakati wa kuondoka kwa MONUSCO nchini humo, ilivyopendekezwa na serikali ya DRC.

Aidha wanachama katika azimio hilo wamesisitiza umuhimu wa kutokomeza vitisho vya usalama vilivyopo bado mashariki mwa nchi, na kufikia mafanikio katika operesheni dhidi ya FDLR.

Kuhusu hilo, Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu nchini DRC, Martin Kobler, ameiambia redio ya Umoja wa Mataifa kwamba MONUSCO iko tayari kushirikiana tena na jeshi la DRC.

« Tunaweza kusaidia jeshi la kitaifa katika operesheni iwapo tu viwango vya haki za binadamu vinaheshimiwa, na hakuna ukiukaji wa haki za binadamu. Haikuwa hivyo hapa, ndiyo maana tulilazimika kusimamisha usaidizi wetu, lakini naamini kwamba tutazirejesha. »

Wakati huo huo, Baraza la Usalama limepitisha azimio la kuongeza idadi ya walinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa zaidi ya 1,000 ili kuimarisha hali ya usalama nchini humo, wakati ambapo nchi inaelekea uchaguzi huku Ufaransa imetangaza kuondoa operesheni yake ijulikanayo kama Sangaris.