Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki za binadamu CAR bado zinatia wasiwasi

Haki za binadamu CAR bado zinatia wasiwasi

Mtalaam huru kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Marie-Thérèse Keita Bocoum ameeleza wasiwasi wake juu ya watu kutoka makundi madogomadogo wanaokumbwa na ukiukaji wa haki za bainadamu.

Akizungumza wakati wa mjadala maalum kuhusu CAR kwenye Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, Uswisi, mtalaam huyo amekaribisha jitihada zilizofanywa na majeshi ya kimataifa ili kurejesha hali ya usalama, lakini amesema bado waasi wanaendelea kutesa raia nje ya mji mkuu Bangui na jeshi la kitaifa linahitaji kuimarishwa.

Kuhusu haki za binadamu , amezingatia ubaguzi wa dini unaokumba watu walio wachache, hasa waislamu ambao wanatengwa na jamii kweney baadhi ya waislamu. .

(Sauti ya Bi. Keita)

“ Mvutano unaweza kuwa mbaya na kuathiri maendeleo ya nchi. Ni lazima vitendo vizingatie ahadi, ili kuelimisha jamii na kuwaeleza kwamba, hata kama watu hawa ni wageni, bado wana haki ya kushirikiana kwenye maendeleo na kufurahia rasimali ya nchi”

Aidha amesikitishwa na ripoti za mateso na mauaji dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya ushirikina.

(Sauti ya Bi Keita)

“ Bila sheria, bila madaraka, watu kadhaa wamejifanya majaji wa jamii na kushtaki watu kwa madai ya ushirikina, kuwatesa, hadi kuwaua, wakati huwa wanawashtaki ili kuwatoza pesa”

Bi Keita amesema ni lazima kupambana na ukwepaji wa sheria na kuendelea na utaratibu wa maridhiano.