Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhuru wa imani au kuabudu kuangaziwa Lebanon

Uhuru wa imani au kuabudu kuangaziwa Lebanon

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kuabudu Heiner Bielefeldt kuanzia tarehe 23 mwezi huu atakuwa na ziara ya takribani wiki mbili nchini Lebanon.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema lengo la ziara hiyo ni kutathmini hali ya uhuru wa kuabudu na imani nyinginezo nchini  humo.

Bwana Bielefeldt amesema ana hamu ya kufahamu zaidi kuhusu uwepo wa pamoja wa jamii zenye imani tofauti nchini Lebanon,  halikadhalika kupata mifano mizuri ya kuigwa.

Pia amesema itakuwa ni fursa kwake yeye kutathmini hali ya uhuru wa kuabudu wa wa imani kwa wakimbizi na wahamiaji.

Akiwa Lebanon, mtaalamu huyo atakutana na viongozi mbali mbali wa serikali, wawakilishi wa jamii kutoka imani mbali mbali za dini, mashirika ya kiraia na yale ya Umoja wa Mataifa.

Matokeo ya ziara yake ikiwemo mapendekezo, atayawasilisha mbele ya Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa katika tarehe itakayopangwa.