Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan yaanza kuwapatia vitambulisho raia wa Sudan Kusini

Sudan yaanza kuwapatia vitambulisho raia wa Sudan Kusini

Serikali ya Sudan imeanza kusajili raia wa Sudan Kusini wanaoishi nchini humo na hivyo kutoa fursa ya wao kupata vitambulisho na kuweza kuajiriwa na kupata huduma za msingi.

Shughuli hiyo imeanza tarehe Mosi mwezi huu kufuatia makubaliano yaliyotiwa saini mwezi Disemba mwaka jana kati ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na mamlaka za Sudan ikiwemo ile inayohusika na hati za kusafiria na uhamiaji.

Hadi sasa zaidi ya raia 54,000 wa Sudan Kusini wamesajiliwa na kati yao 37,000 wamepatiwa vitambulisho.

UNHCR inatoa usaidizi wa kifedha na kiufundi na msemaji wake Adrian Edwards anafafanua..

(Sauti ya Adrian)

“Chini ya makubaliano hayo, raia wa Sudan Kusini waliosajiliwa wenye umri wa zaidi ya miaka mitano wanapatiwa vitambulisho kwa kipindi chote wanachokuwepo Sudan. Kitambulisho hicho kinawapatia haki sawa kama raia wa Sudan na wana haki ya kufanya kazi, kununua rasilimali, kutembea na kuishi popote pale nchini humo.”

Takribani raia Nusu Milioni wa Sudan Kusini wanaishi Sudan na idadi hiyo ni pamoja na raia 120,000 waliokimbia makwao kufuatia mapigano yaliyozuka mwezi Disemba mwaka 2013.