Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 10 ya mkataba wa kudhibiti Tumbaku kuna mafanikio:WHO

Miaka 10 ya mkataba wa kudhibiti Tumbaku kuna mafanikio:WHO

Kuelekea maadhimisho ya miaka 10 hapo kesho tangu kupitishwa kwa mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku, shirika la afya duniani, WHO linasema kuna sababu za kusherehekea kutokana na mafanikio yaliyopatikana dhidi ya bidhaa hiyo inayosababisha janga kwenye afya ya umma. Taarifa zaidi na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Uvutaji sigara au matumizi ya tumbaku hadharani si tena jambo linalokubalika kirahisi katika jamii kama ilivyokuwa awali, na halikadhalika bei ya sigara imeongezwa kwa asilimia 150 kwenye baadhi ya nchi wanachama wa mkataba huo, amesema Mkuu wa sekretarieti ya WHO inayohusika na mkataba huo, Dkt. Vera Luiza da Costa e Silva alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuhusu mafanikio ya mkataba huo ambao hadi sasa umeridhiwa na nchi 180.

(Sauti ya Dkt. Vera)

“Matangazo ya tumbaku na ufadhili unaofanywa na bidhaa hizo umepungua sana, sheria na kanuni za udhibiti zimetungwa na kuimarishwa sehemu nyingi duniani na kuna kampeni nyingi za kuhamasisha dhidi ya tumbaku na kuelezea athari zake kiafya.”

Licha ya mafanikio, harakati zinaendelea ili kuimarisha udhibiti wa tumbaku ambao husababisha vifo vya watu Milioni Sita kila mwaka duniani kote.

(Sauti ya Dkt Vera)

“Sasa hivi tunajadili ufungashaji wa sigara na tumbaku usio na picha na changamoto za sekta ya tumbaku kwa mujibu wa mikataba ya biashara na pia tunajadili mbinu za kupiga marufuku uwekaji hadharani wa bidhaa za tumbaku madukani.”