Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tauni yaua watu 40 Madagascar, WHO yatuma mtaalamu

Mtoto huyu alinusurika baada ya kuugua ugonjwa wa tauni nchini Madagascar.(Picha ya IRIN/Tiana Randriaharimalala)

Tauni yaua watu 40 Madagascar, WHO yatuma mtaalamu

Mlipuko wa ugonjwa wa Tauni nchini Madagascar umesababisha vifo vya watu 40 ambapo shirika la afya duniani WHO limetuma mtaalamu wake kuratibu hatua za kukabiliana na ugonjwa huo. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

WHO imesema kuna hatari kubwa kwa ugonjwa huo unaotokana na vimelea vinavyoishi kwenye mwili wa panya ukaenea kwa kasi zaidi kisiwani humo ambako tayari wilaya 16 za taifa hilo zimeshakumbwa na mlipuko huo.

Mgonjwa wa kwanza alifariki dunia tarehe Tatu mwezi Septemba mwaka huu na vifo vingine vimeripotiwa kwenye mji mkuu Antananarivo, wakati huu ambapo harakati za kudhibiti ugonjwa huo wa Tauni zimekumbwa na mkwamo kwa sababu ya usugu wa vimelea hivyo kwa dawa zinazotumika dhidi yao.  Christian Lindmeier ni msemaji kutoka WHO.

 (Sauti ya Christian)

 "Milipuko ya tauni imekuwa inatokea Afrika, Asia na Amerika ya Kusini, lakini tangu miaka ya 1990 visa vingi vimeripotiwa Afrika. Kile kinachotutia hofu ni kwamba visa vya wakati huu ni vingi zaidi kuliko vilivyokuwepo awali nchini Madagascar.”

 Dalili za ugonjwa wa Tauni zinafanana na zile za homa ya mafua na huchukua siku kati ya tatu hadi saba kwa ugonjwa kujitokeza.