Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uharibifu Mashariki ya Kati ukome na amani ianze: Ban

UN Photo/Amanda Voisard
UN Photo/Amanda Voisard

Uharibifu Mashariki ya Kati ukome na amani ianze: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema anatiwa wasiwasi mkubwa na hali huko Yerusalem na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan akisema vitendo vya uchochezi vinavyohusisha maeneo matakatifu yanachochea moto wa vita mbali zaidi na miji matakatifu.

Ban ametoa kauli hiyo wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya mshikamano na Palestina katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa akitaka uharibifu wa mara kwa mara kwenye maeneo hayo unaotokana na mashambulizi ukome na mchakato wa amani uendelee.

( SAUTI BAN)

“Ninarudia niilchosema Gaza, nalaani mashambulizi ya roketi ya Hamas yanayowalenga bila kubagua raia wa Israeli. Mashambulizi hayo hayajaleta chochote zaidi ya mateso kwa pande zote. Narudia pia nilichosema Israel, kiwango cha uharibifu wa jeshi la Israel kimetuacha na maswali mengi mazito kuhusu heshima kwa kanuni za kutofautiana na uwiano, na kuibua wito wa kutaka uwajibikaji.”

Akihutubia kikao hicho Rais wa Baraza Kuu, Sam Kutesa amesema hali Mashariki ya Kati ni tete huku hali ya Yerusalem na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan vikisalia kuwa chanzo kikubwa cha matatizo.

Bw Kutesa ametoa wito kwa pande zote ziwe tulivu na kujizuia sambamba na kujiepusha na vitendo vya uchochezi.

Kuhusu nafasi ya Umoja wa Mataifa ya kupatikana kwa amani ya kudumu, Kutesa amesema.

(SAUTI KUTESA)

“Wakati huu ni mwafaka hasa kwa Umoja wa Mataifa kuchukua jukumu kubwa, katika kusaidia pande zote katika mgogoro ili zifikie suluhu ya kina na ya haki katika Mashariki ya Kati. Majadiliano ni lazima yajikite katika ufumbuzi wa uwepo wa mataifa mawili ya Israeli na Palestina yanayokuwepo kwa amani na usalama na katika mipaka inayotambuliwa”