Wahudumu wa afya wanaotibu Ebola wasinyanyapaliwe wanaporejea- WHO

28 Oktoba 2014

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema kuwa ni mapema mno kusema ikiwa vikwazo kwa wahudumu wa afya wanaorejea kutoka nchi zilizoathiriwa na Ebola kutawafanya wengine wasitake kwenda Afrika Magharibi kusaidia katika kupambana na tatizo la Ebola.

Jimbo la New Jersey ni moja ya majimbo matatu Marekani ambayo yameweka karantini ya siku 21 kwa wahudumu wote wa afya ambao wamewagusa wagonjwa wa Ebola. Jimbo hilo limekataa kubadili sera yake ya karantini licha ya mwongozo mpya wa kitaifa nchini Marekani, ambao unasema kuwa madaktari wa Marekani wanaorejea kutoka kuwatibu wagonjwa wa Ebola Afrika Magharibi watafuatiliwa kwa karibu lakini hawatawekwa karantini. Uamuzi huo ulifuatia hatua ya muuguzi mmoja kuwekwa karantini kwa hema katika jimbo la New Jersey, hatua ambayo imewaghadhabisha wanasiasa na wahudumu wa afya.

Australia pia imeshutumiwa kwa kupiga marufuku utoaji wa visa kwa watu wanaotoka Afrika Magharibi.

WHO haipendekezi karantini ya lazima. Tariq Jasarevic ni msemaji wa WHO

“Ni muhimu kulinganisha hatua zozote zinazochukuliwa, kati ya kile kinachochukuliwa kama kulinda umma na hatari ya unyanyapaa. Tunahitaji wahudumu wa kimataifa kwa dharura. Wao ni sehemu muhimu ya mapambano, na watu hawa wanaporudi nyumbani, wasifanyiwe vitendo vya kunyanyapaliwa.”

Hapo jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alisema kuwa wahudumu wa afya wanaorejea kutoka Afrika Magharibi ni watu jasiri wanaojitoa kwa ajili ya ubinadamu, na kwamba wasiwekewe vikwazo ambavyo havitokani na misingi ya kisayansi.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter