Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ISIL waharibu sehemu za ibada nchini Syria- Ofisi ya Haki za Binadamu

Mjini Aleppo - Syria, picha ya UNESCO

ISIL waharibu sehemu za ibada nchini Syria- Ofisi ya Haki za Binadamu

Kundi la waasi waislamu wenye msimamo mkali ISIL, linadaiwa kubomoa sehemu za ibada na majengo ya urithi wa utamaduni wa dunia nchini Syria.

Mmsemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu Rupert Colville, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa mapigano kati ya jeshi la serikali na ISIL yamesababisha uharibifu mkubwa wa sehemu za ibada nchini Syria, pande zote zikiripotiwa kuhusika katika uharibifu wa makanisa, miskiti na sehemu za kihistoria.

Colville amesema ofisi ya haki za bonadamu inalaani vikali kubomolewa kwa kanisa la Kiarmenia na ISIL mwezi uliopita, akielezea pia wasiwasi wake juu ya hatma ya mapadri watatu waliotekwa nyara tangu mwaka jana.

Amesema sheria ya kimataifa ya kibinadamu inaweka kipaumbele majengo ya ibada na viongozi wa kidini.

Hatimaye ameleza kwamba uhalifu unaotekelezwa na ISIL hauna msingi wowote wa kidini:

“ Wakiua watu kwa msingi wa kuamua wenyewe kwamba si waislamu wa ukweli au wameasi dini, wanajidai kuhudumia dini ya kiislamu. Lakini kwa ukweli wanataka tu kuongeza utawala wao kwa kutisha watu. Ndio maana ISIL inabomoa pia miskiti ya Wasunni, inaua Wasunni, wanawake na watoto, hata maimamu Wasunni. Yaani kila mtu asiyekubali msimamo wao mkali wa kidini yuko hatarini”