Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya watu kuandamana New York kuhusu tabianchi

Maelfu ya watu kuandamana New York kuhusu tabianchi

Makumi ya maelfu ya watu wanatarajiwa kuandamana katikati mwa jiji la New York leo Jumapili kuteta dhidi ya jamii ya kimataifa kupuuza kuchukua hatua za kukomesha mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon anatarajiwa kujiunga na wanasiasa, watu mashuhuri, wanaharakati na raia wa kawaida katika maandamano hayo ya kumulika hofu iliyopo ulimwenguni kuhusu hatari za mabadiliko ya tabianchi.

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na kufurika kwa kimo cha maji baharini, majanga ya hali ya hewa na ongezeko la joto.

Maandamani ya tabianchi leo yanafanyika siku mbili tu kabla ya mkutano wa Katibu Mkuu kuhusu tabianchi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Mkutano huo utawaleta pamoja zaidi ya viongozi wa nchi 120, ili kuweka msukumo wa kufikia mkataba wa kimataifa kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Inatarajiwa kuwa mkataba huo utafikiwa mjini Paris, Ufaransa hapo mwakani.