Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi mengine Yemen yasababisha watu kukimbia makwao

Picha ya OCHA - Yemen

Mashambulizi mengine Yemen yasababisha watu kukimbia makwao

Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA imesema mashambulizi yaliyoibuka tena katika mkoa wa Al Jawf, kaskazini mwa Yemen, yamesababisha familia nyingine kukimbia makwao.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema familia 1500 zimekimbia tangu mwisho wa Julai, idadi hii ikiwa ni ndogo kwani watu karibu wote wameshakimbia eneo hilo, ambalo kwa kawaida halina makazi mengi.

Dujarric ameongeza, familia 300 zimekimbia makwao kwenye eneo la Marib ambapo mapigano yamerejea tangu juzi, lakini mashirika ya kimataifa hayajaweza kuwafikia watu hao kwa sababu ya ukosefu wa usalama.

Kwa mujibu wa ripoti ya OCHA iliyotolewa mwisho wa Agosti mwaka huu, idadi ya wakimbizi wa ndani nchini Yemen imefikia 335,000, pamoja na wakimbizi 245,000 kutoka Somalia, OCHA ikisema kwamba ukosefu wa usalama na mapigano ya mara kwa mara yanakwamisha usambazaji wa misaada.