Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahusika wa ukatili Cambodia wafungwa kifungo cha maisha

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi mahakama, Cambodia.Picha ya UM/NICA/maktaba

Wahusika wa ukatili Cambodia wafungwa kifungo cha maisha

Nchini Cambodia mahakama maalum inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imewahukumu kifungo cha maisha wahusika wawili wa vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu vilivyofanyika miaka ya sabini nchini humo. John Ronoh na taarifa kamili.

 (Taarifa ya John)

Jopo la majaji wa mahakama hiyo maalum limeamua kuwa Nuon Chea na Khieu Samphan wana hatia ya kutekeleza uhalifu dhidi ya ubinadamu kati ya Aprili mwaka 1975 na Disemba 1977, na hivyo kuwahukumu wote kifungo cha maisha. Hukumu imesomwa na Jaji Nill Nonn, rais wa jopo hilo la majaji.

(Sauti ya Jaji Nill)

 "Mahakama hii imewakuta washatakiwa na hatia ya kutekeleza uhalifu dhidi ya ubinadamu, ukijumuisha mauaji, kuuwa kwa misingi ya kisiasa na vitendo vingine dhidi ya ubinadamu ikiwemo, kuhamishwa watu kwa lazima, kulazimishwa kutoweka na ukiukaji wa ubinadamu nchini Cambodia kati ya Aprili mwaka 1975 na Disemba 1977. Mahakama hii imemhukumu Nuon Chea kifungo cha maisha. Mahakama hii imemhukumu mshatakiwa Khieu Samphan kifungo cha maisha."

Khieu Samphan alikuwa kiongozi wa kijeshi na Nuon Chea alikuwa Naibu Katibu wa Chama cha Kikomiunisti cha Kampuchea, na mwanachama wa kamati kuu za utawala.

Shughuli hizo zilitekelezwa kwa kuwafurusha watu wote wa Phnom Penhkutoka mijini na vijijini mwao kwa lazima, na hivyo kuwahamisha watu wapatao milioni mbili kwa kutumia utesaji, vitisho vya bunduki, huku wanajeshi wa Khmer Rouge wakiwaua watu wengi.