Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amteua Mary Robinson kuwa Mjumbe Maluum wa mabadiliko ya tabianchi

Bi Mary Robinson Picha@UM

Ban amteua Mary Robinson kuwa Mjumbe Maluum wa mabadiliko ya tabianchi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, leo ametangaza kumteua Bi Mary Robinson wa Ireland kuwa Mjumbe wake Maalum kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Bi Robinson ataendelea kuhudumu kama rais wa wakfu wake wa Climate Justice.

Kutokana na uzoefu katika kazi ya wakfu wake, Bi Robinson anatarajiwa kusisitiza mtazamo unaowajali watu katika mikakati inayojikita kwa mabadiliko ya tabianchi, huku akishirikiana na wajumbe wengine kama John Kufuor na Michael Bloomberg katika kuchagiza utashi wa kisiasa na uchukuaji hatua kabla ya mkutano kuhusu tabianchi wa tarehe 23 Septemba 2014.

Bi Robinson atairithi nafasi ya Jens Stoltenberg wa Norway, ambaye karibuni ameteuliwa Katibu Mkuu wa Shirika la Mkataba wa Kaskazini mwa Atlantiki, NATO.

Akitangaza uteuzi huo wa Bi Robinson, ambaye pia amekuwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu kuhusu nchi za ukanda wa Maziwa Makuu, Ban amempongeza kwa kazi yake kama Mjumbe Maalum kwa Ukanda wa Maziwa Makuu ya Afrika, hususan katika juhudi zake za kuleta utangamano na uelewa wa kimataifa kwa matatizo ya ukanda wa Maziwa Makuu.