Skip to main content

Mkuu wa usalama UNSOM azungumzia mchango wa wanawake katika ulinzi wa amani

Bendera ya Somalia picha ya UNSOM

Mkuu wa usalama UNSOM azungumzia mchango wa wanawake katika ulinzi wa amani

Mkuu wa idara ya usalama katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Olga Mokrova, amesema kuwa wanawake wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za ulinzi wa amani, kutokana na sifa zao za asili, na kwa hiyo wanawake zaidi wanatakiwa kuwa katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa ulinzi wa amani.

Bi Bokrova amesema hayo katika mahojiano maalum na Redio ya Umoja wa Mataifa, siku mbili kabla ya Siku ya Walinda Amani Duniani, Mei 29. Bi Bokrova ameeleza ni kwa nini wanawake wanatakiwa wawe katika ujumbe wa ulinzi wa amani

Wanawake wana sifa mbili za asilia ambazo ni huruma, na pia wana uwezo wa kutambua vitu vingi vilivyo katika mazingira yao. Matatizo mengi katika nchi zinazoibuka kutoka mizozoni yanahusu wanawake, watoto kuingizwa jeshini, na uwezo wa wanawake katika ujenzi wa amani na kutafutia suluhu matatizo mengi yanayohusika na mizozo, hauwezi kupuuzwa. Nadhani Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Somalia ni mfano mzuri ambako kuna usawa wa jinsia kwani idadi kubwa ya wanawake hapa wanaongoza idara nyingi”

Hata hivyo, ameonya kuwa wasichukuliwe tu wanawake wowote wale kwa minajili ya kuajiri wanawake wengi zaidi kuliko wanaume, ila wanatakiwa wawe na weledi ufaao katika kutekeleza majukumu wanayohitajika kuyatekeleza.

Tunatakiwa kuwachukuwa wanawake bora zaidi, ambao wamebobea kielimu na kitaaluma, na wenye uzoefu wa kufanya kazi katika mazingira yenye watu wa asili tofauti, kwani ukifikiria kuhusu majukumu ya kulinda amani, haya ni majukumu yanayoweza kuwa hatari mno.”