UNICEF yalaani mashambulizi dhidi ya watoto Syria

30 Aprili 2014

Wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, likikutana kujadili hali nchini Syria, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limetoa taarifa ya kulaani mashambulizi dhidi ya watoto nchini Syria. Joshua Mmali na taarifa kamili

TAARIFA YA JOSHUA

UNICEF imeelezea kusikitishwa na wimbi la hivi karibuni la mashambulizi ya kiholela yanayotekelezwa dhidi ya mashule na maeneo mengine ya raia kote nchini Syria, ambayo yamewaua watoto wengi na kuwajeruhi wengine.

Hapo jana Jumanne, Aprili 29, kulishuhudiwa mashambulizi matatu, moja likiwa kwenye kitongoji cha Al-Shaghour mjini Damascus na jingine kwenye taasisi ya kitaaluma ya Badr Al Din Hussein. Ripoti zinasema kuwa watoto 14 waliuawa na zaidi ya 80 wengine kujeruhiwa.

Shambulio jingine la kombora lilifanyika kwenye kijiji cha A’dra, Damascus, likiripotiwa kuwaua watoto watatu. Mjini Homs bomu lilipuliwa kwenye gari na kuwaua watu wapatao 100, wakiwemo wanawake wengi na watoto, na kuwajeruhi zaidi ya watu 100.

Hii leo Baraza la Usalama linakutana kuhusu hali nchini Syria, na kusikiliza ripoti ya Mratibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Matataifa, OCHA, Bi Valerie Amos kuhusu misaada ya dharura nchini humo.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter