Mtaalamu wa UM ametolea wito mamlaka za Kazakhstan kusitisha usajili wa jamii za kidini

4 Aprili 2014

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa Heiner Bielefeldt ametolea wito serikali ya Kazakhstan kusitisha  usajili wa lazima wa jumuiya za kidini kwani hali hiyo imezua hofu ya ukosefu wa usalama wa kisheria na kuathiri makundi madogo ya watu.

Amesema kwamba uwepo wa madhehebu mbali mbali ya kidini ni wa siku nyingi katika  historia ya jamiiKazakhstan.

Bwana Bielefeldt alisema hayo baada ya ziara yake ya kwanza kabisa nchini humo akiwa mtaalamu huru aliyeteuliwa na Umoja wa Mataifa kuchunguza uhuru wa kuabudu. Amesema baadhi ya watu aliozungumza nao walionyesha uwazi wa kukubali watu wa jamii za dini tofauti nchini Kazakhstan.

Hata hivyo sheria ya 2011 kuhusu muungano wa dini inapendekeza usajili wa jamii zote za kidini nchini Kazakhstan ili kuweza kuendesha shughuli za kidini. Mtaalamu huyo amesema wale ambao hawajisajili wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa kisheria na hivyo kuathiri uhuru wao wa kuabudu. Amesisitiza kuwa uhuru wa kuabudu au imani ni haki ya kila binadamu na hauhitaji kupitishwa na serikali