Wananchi wamechoka na vita, wanatoa taarifa za uhalifu CAR: UM

4 Aprili 2014

Wakati ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imetembelea manusura wa tukio la mashambulizi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambapo kundi la Anti Balaka liliwashambulia askari walinda amani kutoka Chad, mwenyekiti wa tume ya kimataifa ya uchunguzi Benard Muna amesema watu wa CAR wamechoka na machafuko nchini humo.

Taarifa zadi na Joseph Msami

Katika mahojiano maalum na Jean Pierre Ramazani wa radio ya UM Bwana Muna anayechunguza matukio ya uvunjifu wa sheria za kimataifa za utu, haki za binadamu na aimba nyingine za uhalifu amesema wanapata taarifa kutoka kwa wananchi walioko pembezoni, mashirika na jumuiya ya kimataifa kuhusu matukio mbalimbali.

Amesema taarifa hizo zitakuwa msaada mkubwa katika kutimiza lengo la uchunguzi wa matukio ya uhalifu ili sheria ichukue mkondo wake

"Kuna raia wengi wa nchi hii ambao wamechoka na machafuko, wako nje ya mji wa Bangui na wanatupa taarifa, mashirika ya UM yanakusanya taarifa, asasi za kiraia pia. Taarifa hizi zitatusaidia kuchunguza na kufikia hitimisho la majukumu tuliyopewa na UM hususani baraza la Usalama".

Mteule huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anaamini kazi ya tume yake itakamilika na kutenda haki kwa ajili ya mustakabali mwema wa Jamhuri ya Afrika ya Kati